WATUMISHI 6 KALIUA WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UPOTEVU WA MIL.119

Halmashauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imewafikisha Mahakamani watumishi wake 6 kwa tuhuma za upotevu wa fedha za mapato kiasi cha sh.milioni 119 walizokusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato.. Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Dkt.John Pima wakati wa hafla ya kukabidhi mashine mpya 43 za kukusanyia mapato kwa watendaji […]

Halmashauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imewafikisha Mahakamani
watumishi wake 6 kwa tuhuma za upotevu wa fedha za mapato kiasi cha
sh.milioni 119 walizokusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali vya
mapato..

Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo
Dkt.John Pima wakati wa hafla ya kukabidhi mashine mpya 43 za
kukusanyia mapato kwa watendaji wa vijiji na kata ambazo zinafanya
idadi kamili ya mashine hizo kufikia 69.

Dkt.Pima alisema kuwa agenda ya ukusanyaji mapato ni ya kitaifa na
kila mtumishi wa halmashauri aliyepewa dhamana ya kukusanya mapato
anatakiwa kutekeleza wajibu wake kwa weledi na uaminifu, kinyume na
hapo sheria itachukua mkondo wake.

Alifafanua kuwa mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano ni mapato kwanza
ndio maana serikali ilitoa mashine za kukusanyia mapato na sasa imetoa
mashine nyingine tena ili kuhakikisha kila halmashauri inakusanya
mapato ya kutosha.

Alibainisha kuwa kila fedha ya mapato inayokusanywa kutoka katika
vyanzo vya ndani inapaswa kuwasilishwa benki na mtumishi husika na
yeyote anayetumia fedha hiyo kinyume na utaratibu hatua kali lazima
zichuliwe dhidi yake.

“Tumebaini kuwa sh.milioni 119 za mapato hazijulikani zilipo na
watumishi 6 waliohusika na upotevu huo tumewachukulia hatua za
kinidhamu ikiwemo kufikishwa mahakamani ili sheria ikafuate mkondo
wake” alisema.

Alieleza kuwa hadi kufikia Disemba mwaka jana halmashauri hiyo ilikuwa
imekusanya sh. bilioni 1.3 sawa na asilimia 54 ya makisio yake ya
kukusanya sh bil 3.2 za bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020, hivyo wana
uhakika wa kuvuka lengo, aliagiza kila mtumishi kutimiza wajibu wake
ipasavyo.

Akiongea katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa wilaya Abel Busalama
Katibu Tawala wa wilaya hiyo Michael Nyahinga aliwataka watumishi wote
wa halmashauri waliokabidhiwa mashine hizo kuzitumia ipasavyo kwa
lengo lililokusudiwa.

Alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John
Pombe Magufuli haitaki mchezo katika suala la ukusanyaji mapato, hivyo
yeyote atakayeleta ujanja ujanja katika mashine hizo atachukuliwa
hatua kali ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Kwa upande wake  Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA
wilayani hapa Denis Gaspar alionya kuwa mashine hizo zimeunganishwa
kwenye mfumo maalumu na zina mtandao masaa 24 hivyo zinapaswa kuwa
hewani wakati wote, zisizimwe.

0 comments

Online Shopping in BangladeshCheap Hotels in Bangladesh