Bunge limeazimia kwamba Serikali itumie Taasisi ya Umma ya Wakala Mtandao (E – Government)

Bunge limeazimia kwamba Serikali itumie Taasisi ya Umma ya Wakala Mtandao (E – Government) kusimamia na kuratibu shughuli zinazoendelea za uwekaji mifumo ya Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA). Ushauri huo ulitolewa bungeni jana na Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC), Naghenjwa Kaboyoka wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati kwa mwaka […]

Bunge limeazimia kwamba Serikali itumie Taasisi ya Umma ya Wakala Mtandao (E – Government) kusimamia na kuratibu shughuli zinazoendelea za uwekaji mifumo ya Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA).

Ushauri huo ulitolewa bungeni jana na Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC), Naghenjwa Kaboyoka wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati kwa mwaka 2019 ambayo imeanisha changamoto na dosari mbalimbali yaliyojitokeza katika Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Aidha, alisema jambo hilo litasaidia kuweka uwajibikaji na kupunguza gharama ambazo Serikali imekwishaingia hadi sasa.

Alieleza kuwa kamati inamuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kadri atakavyoona inafaa, kufanya ukaguzi wa ufanisi wa shughuli zinazohusu ununuzi na usimikaji wa mifumo katika Taasisi za Umma.

Alisema kuwa ukaguzi huo utakuwa muhimu ili kutoa mwongozo na ushauri kwa Taasisi za Umma katika manunuzi ya mifumo ili kuepuka gharama zisizo za lazima kwa siku zijazo.

Kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), alisema kwa kuwa taarifa ya CAG imebainisha kutokuwepo kwa makubaliano ya kimaandishi ya mkopo  wa shilingi 82,736,176,217 kati ya NHIF na Chuo Kikuu Dodoma kuhusiana na ujenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, pamoja na kupungua kwa hali ya mtaji wa Mfuko.

Alisema kutokuwepo kwa makubaliano hayo ni dosari ya kiuhasibu katika Hesabu za Mfuko, na pia kupungua kwa hali ya mtaji kunaathiri uwezo wa kifedha wa Mfuko kutekeleza wajibu wake wa Kisheria.

Kutokana na hali hiyo alisema Bunge linaazimia kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF na Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya Benjamini Mkapa wafuatilie kwa karibu Serikalini suala la makubaliano ya kimaandishi ya mkopo wa ujenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa ili kufunga hoja husika.

Kuhusu mtaji wa mfuko, kamati iliitaka NHIF ihakikishe kunakuwepo mwenendo mzuri wa Mfuko, kwa kuongeza udhibiti na ufuatiliaji wa kiwango cha madai ya huduma ili kuepuka madai hewa ambayo yanaathiri shughuli za Mfuko.

Aidha, NHIF iendelee kufanya tafiti mbalimbali za kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwekeza asilimia fulani ya michango ya wanachama ili uwekezaji huo uje kusaidia malipo ya huduma za afya kwa wanachama pindi watakapostaafu.

Kuhusu Utendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), alisema kwakuwa taarifa ya Ukaguzi katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imebainisha dosari kubwa za kiutendaji ikiwa ni pamoja na CAG kutoa “ disclaimer of opinion” katika Hesabu za Shirika.

Alieleza kuwa dosari hizo zimesababisha Serikali kutopata faida stahiki kama gawio na kodi balimbali kutoka kwa STAMICO na Kampuni zake Tanzu.

“Bunge linaazimia kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Msajili (TRO) wa Hazina iimarishe usimamizi wa karibu wa STAMICO ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya shughuli za utendaji wa kila siku wa Shirika hilo,”alisema.

Pia, Serikali ifanye mapitio ya Mikataba yote ambayo STAMICO imeingia na Kampuni Tanzu ili kuhakikisha makubaliano katika Mikataba yanatekelezwa ipasavyo na masharti hasi yanaondolewa.

Kaboyoka alisema STAMICO ifanye uthamini wa mali zake ili kutambua thamani halisi ya mali za Kampuni kwa sasa.

Kuhusu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), alisema taarifa ya CAG imebainisha uwepo wa Miradi mingi iliyo chini ya NHC ambayo imeshindwa kukamilika kwa wakati   kutokamilika kwa Miradi hiyo kumeongeza gharama za ujenzi na kuisababishia Serikali hasara kubwa, kutopatikana kwa thamani halisi ya fedha iliyowekezwa na pia kuwepo kwa uwezekano wa NHC kushtakiwa na Wakandarasi.

Alisema bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie namna bora ya kuiwezesha NHC kukamilisha Miradi ambayo ilikuwa katika hatua za mwisho za utekelezaji ili kupunguza hasara ambayo tayari imepatikana.

Aidha,  Serikali iendelee na uchunguzi wa kina wa Miradi yote ya NHC ili kubaini dosari zilizopo katika Miradi husika. Baadhi ya Miradi imebainika kuwa ilitekelezwa kwa gharama zisizo halisia na usimamizi wake haukuwa na ufanisi.

kuhusu, kutokamilika kwa wakati kwa Miradi ya Wakala wa Majengo Nchini(TBA) alisema kamati imebainisha hali ya kutokamilika kwa wakati kwa Miradi inayotekelezwa na TBA hapa Nchini.

Alifafanua kuwa kutokamilika kwa Miradi hiyo kunaisababishia Serikali hasara kwa kuongeza gharama za ujenzi na kuwanyima Wateja fursa za kutumia Miradi husika kwa wakati mwafaka.

“Bunge linaazimia kwamba TBA waboreshe na kuimarisha Kitengo cha usimamizi wa utekelezaji wa Miradi ili kuhakikisha miradi yote inaanza na kukamilika kwa kuzingatia muda uliokubalika Kimkataba,”alisema.

Aliitaka TBA wabuni utaratibu wenye ufanisi wa udhibiti wa mifumo ya ndani katika utekelezaji wa Miradi hasa katika eneo la matumizi ya fedha, vifaa vya ujenzi na rasilimali watu ili kuharakisha utekelezaji wa Miradi.

Kuhusu, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Uchambuzi wa Kamati katika Taarifa ya CAG ulibaini kuwa uwekezaji wa NSSF katika hisa za Vodacom haukuzingatia mwongozo wa Uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii;

Alisema uwekezaji huo unatoa riba ndogo kuliko riba inayotolewa na dhamana za Serikali hivyo kuikosesha NSSF mapato stahiki hivyo Bunge linaazimia kwamba, Serikali ifanye uchunguzi wa kina wa suala hili na kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi.

Kuhusu, usimamizi wa Mikataba ya Ujenzi katika Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia
alisema kamati imebaini mapungufu katika usimamizi wa shughuli za ujenzi na ukarabati wa vyuo vya Ualimu unaotekelezwa katika Fungu – 46 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Alieleza kuwa mapungufu hayo yamesababisha ongezeko la gharama za ujenzi na hivyo kuisababishia Serikali hasara na pia kutofikiwa kwa malengo ya Wizara hivyo Bunge linaazimia kwamba wizara hiyo iimarishe Kitengo cha usimamizi wa Mikataba ya ujenzi na ukarabati.

Aidha, majengo yote ambayo yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi yakamilike na taarifa zitolewe kwa CAG.

You may also like

0 comments

Online Shopping in BangladeshCheap Hotels in Bangladesh